DIAMOND NDO SUKARI YAO...WEWE MAMA WEMA, BADO TU HAUJIFUNZI?

Mama mzazi wa Wema Sepetu, Miriam Sepetu
HII ni mara yangu ya tatu nazungumza na mama mzazi wa Wema Sepetu, Miriam Sepetu juu ya mwenendo wake kwa mwanaye, ambaye ana simulizi nyingi zinazomhusisha na mambo yaliyo nje ya fani yake ya uigizaji.
Wakati ule, ilikuwa ni juu ya tabia yake ya mara kwa mara ya kulizungumzia penzi la Wema na Diamond, kabla wawili hao hawajaachana kwa mara ya kwanza. Alikuwa akimpinga waziwazi kijana yule wa Tandale, kwa madai kuwa anampotezea muda mwanaye na mambo mengine kama hayo.
Nilijaribu kumweleza kwa jinsi gani ilikuwa haipendezi kwake kufuatilia sana mambo ya kimapenzi kwa watoto, maana ingawa anayo nafasi kubwa, lakini aina ya maisha ya siku hizi yanatoa nafasi kubwa zaidi kwa wahusika kuliko wazazi.
Lakini wakati akijipongeza kwa kufanikisha kuachana kwa wawili hao, ghafla wakarudiana na kumfanya mama mtu kuaibika, kwani ilionyesha wazi mwanaye alikuwa bado ana mapenzi kwa Baby wake, Diamond Platinumz.
Na mara ya pili nilisema naye wakati alipomtukana matusi makubwa ya nguoni shoga wa zamani wa mwanaye, Kajala Masanja, katika sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mtoto wake. Ni matusi ambayo licha ya kuwa hayaandikiki gazetini, lakini pia nilimweleza jinsi gani alivyokosa busara za mzazi kwa kutamka maneno mazito kama yale, mbele ya watoto!
Safari hii, amerudia tena kosa ambalo nina uhakika, kwa tabia za mtoto wake, linaweza kumkuta akiabika tena kwa mara nyingine. Baada ya taarifa za kutengana tena kwa Wema na Diamond, mama huyu anaripotiwa kuwaalika marafiki zake kisha ‘kuangusha’ pati kushangilia kitendo hicho huku akikiri mbele ya magazeti kwamba ni kweli alifanya hivyo na kwamba, eti Diamond atajiju kwani hana hadhi ya kuwa na mwanaye.
Sina uhakika kama kuna jambo lolote baya ambalo Diamond amemfanyia mama huyu, isipokuwa tu huenda kwa kuwa inatokea, mtu akawa haziivi tu na mwingine, hata ukimuuliza sababu za msingi za kumchukia, huwa hana.
Nilimwambia wakati ule, ni vigumu sana mtu kufanikiwa kuingilia mapenzi ya watu wengine, hasa kama wamependana wenyewe kwa sababu zao. Simsemi vibaya Wema, lakini historia yake ya kimapenzi haimpi uhakika wa kuaminiwa hata kidogo. Ninamfahamu kitambo huyu bibie. Ana orodha ya kuvutia kidogo ya kutoka na mastaa, kama Kim Karadashian wa Marekani, mke wa Kanye West.
Mr Blue, TID, Hartman Mbilinyi, Jumbe Yusuf, Chaz Baba, marehemu Steven Kanumba na Diamond ni miongoni mwa mastaa ambao Wema Sepetu ametoka nao, ukiachana na wengine, (sina uhakika kama ni wengi) ambao mimi na wewe hatuwafahamu.
Huenda anaonekana kama mwenye orodha ya kusisimua ya wanaume kwa sababu ya ustaa wake, lakini wapo pia wanawake wengi tu mtaani ambao nao wanatisha. Alipoachana kwa mara ya kwanza na Diamond, maneno mengi sana yalizungumzwa, siyo tu na yeye mwenyewe, bali pia na wapambe wake.
Ilionekana kama vile ni vigumu sana kwa wawili hao kuwa tena pamoja, lakini picha lilipoanza kuchezwa kule China, hakuna aliyeamini kama ingeishia kwa wao kutambulishana rasmi pale katika Viwanja vya Leaders.
Leo tunaambiwa wameachana. Sijui. Nayajua maisha ya mastaa kwa sababu nimewahi kuwa nao, hawaaminiki, hasa katika eneo hili la mapenzi. Halitakuwa jambo la ajabu kesho na keshokutwa kusikia wawili hawa wamerejesha uhusiano wao, hasa kwa vile wote wameteka masoko ya fani zao.
Wema anaburuza soko la filamu kama ambavyo Diamond hakamatiki katika Bongo Fleva. Kibiashara, hii ni couple ambayo kila mtangazaji angependa kuitumia. Na ukichunguza sababu zilizomfanya Mbongo Fleva huyo kumuacha muigizaji wakati ule, hazina tofauti na zile zinazotolewa safari hii.
Ushauri wangu kwa mama Wema ni kuwa, pamoja na kwamba ni mwanaye lakini sidhani kama anapaswa kumuamini katika eneo hili. Huyu binti bado anakula ujana, akae kimya, amuunge mkono kimyakimya!

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »