Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji huo Novemba 8, mwaka huu katika Hospitali ya John Hopkins iliyopo Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, mastaa wamesema wameguswa na kuumwa huko kwa rais lakini wameshukuru kwamba upasuaji umefanyika salama hivyo wanamuombea apone haraka ili aweze kurudi katika afya yake ya kawaida.
“Mungu asaidie upone haraka baba…tunaumwa nawe,” aliandika Aman Temba ‘Mh. Temba’ mtandaoni huku Esterlina Sanga ‘Linah’ akiandika:“Furaha ya moyo wangu inakamilika na mengi lakini kubwa kuliko yote ni kuona tabasamu lenye afya na uzima tele kwako baba, shujaa rais wangu. Get well soon my shujaa.”
Mbali na wasanii hao, wengine walioonesha kuguswa na kuumwa kwa rais na kuandika hisia zao ni Diamond, Linex, Wolper, Shetta, Shilole na MwanaFa.Mbali na wasanii wananchi mbalimbali wa kawaida kwa nyakati tofauti walieleza hisia zao kupitia gazeti hili: “Nilipopata tu taarifa kwamba mheshimiwa rais amefanyiwa upasuaji, nilishtuka kidogo lakini baada ya hapo mimi pamoja na wenzangu tukafanya maombi maalumu ya kumuombea rais wetu aweze kupona haraka na kuendelea na majukumu yake ya kawaida.
“Niwaombe Watanzania wote tuungane kwa pamoja kumuombea rais wetu maana maombi yetu yana maana kubwa mbele za Mungu,” alisema Mazula, mkazi wa Tabata.
Tezi dume ni nini?
Tezi dume ipo kwa binadamu wa kiume ambapo ina muonekano kama wa yai (oval shape) na upana wake huwa ni CM4 na unene CM3 ingawa kwa mujibu wa madaktari, vipimo hivyo vinatofautiana kwa kila mwanaume.
Tezi dume inazunguka shingo ya kibofu cha mkojo na kuzunguka mrija unaopeleka mkojo nje, kwa kawaida tezi hii ina umbo la wastani na huongezeka ukubwa kadri umri wa mtu unavyozidi kuongezeka.