PANYA ROAD WAFUNGA MITAA MINNE JIJINI DAR ES SALAAM


Ilikuwa hekaheka iliyosababisha shughuli katika mitaa minne ya Tabata, Dar es Salaam kusimama kwa saa nne baada ya kundi la vijana wenye nondo, mawe na visu kushambulia watu, kupora na kuharibu mali kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kulipiza kisasi. 
 
Kundi hilo la vijana zaidi ya 30 ambalo mmoja wao ameuawa linalofananishwa na lile la Panya Road ambalo hivi karibuni lilisumbua jijini Dar es Salaam, liliamua kufanya vurugu hizo Jumamosi na Jumapili baada ya ugomvi kutokea baina ya makundi mawili tofauti.
 
Makundi yaliyohusishwa na ugomvi huo moja ni la Tabata Kimanga, Mtaa wa Magengeni na jingine la Tabata Kisiwani, Mtaa wa Twiga.
 
Chanzo cha vurugu hizo zinaelezwa kuwa ni kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Alfa Mhanga, Mkazi wa Tabata Kisiwani kupigwa na kunyang’anywa simu na wenzake wa kundi jingine.
 
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisiwani, Herbert Haule alisema vijana hao waliingia mitaani na kujeruhi watu, kuiba na kuharibu mali walipokuwa wakilipiza kisasi baada ya mwenzao kupigwa.
 
Hata hivyo, Mkazi wa Kisiwani, Mwita Manofu alisema sakata zima la mkasa huo lilianza Jumamosi wakati vijana wawili waliokuwa wakiangalia mpira kuzozana hadi kupigana na mmoja wa vijana hao kwenda kutoa taarifa kwa kundi lake ambalo lilikuja kulipa kisasi.
 
“Unajua mmoja wa wale vijana alipopigwa alikwenda kuwaita watu wa kundi lake ambao walikuja na kuanza kuwatafuta wa kundi jingine na kuanza fujo ambazo ziliendelea hadi wakaanza kulipa kisasi kwa watu wa mtaani kwa kuwapiga,” alisema.
 
Mama wa kijana mmoja aliyekuwa anatafutwa na vijana hao, Hadija Mhenga alisema: “Vijana zaidi ya 30 wakiwa na mapanga, visu na marungu walikuja hapa saa sita usiku na kuanza kupiga kelele huku wakitaka kuchoma nyumba moto,”alisema.
 
Kijana mwingine, kinyozi katika saluni iliyopo Uwanja wa Twiga, Gerald Manase alisema kundi la vijana kutoka Tabata Kisiwani liliwakodi vijana kutoka Mabibo na Kigogo kuja kulipa kisasi kwa kupiga watu na kuwakata mapanga.
 
Askari mwandamizi wa Kituo cha Polisi Tabata Kisiwani alisema mapambano hayo yaliendelea Jumapili na ndipo kijana mmoja alipouawa.
 
“Kijana aliyeuawa anatokea Mabibo, si mwenyeji wa hapa Kisiwani, aliuawa baada ya wananchi kuwakimbiza vijana hao na kumshika mmoja na kumpiga hadi kufa,” aliongeza kijana Manase.
 
Polisi Tabata Kisiwani walisema vurugu hizo zimedhibitiwa na vijana kadhaa wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa.


Shughuli zasimama
Juzi, taarifa za uvamizi mpya zilisambaa mitaani na kuwafanya wananchi kuanza kujihami kwa kufunga maduka, nyumba na biashara zote zinazofanyika katika mitaa husika.
 
Wakazi wa mitaa ya Mandela Juu, Tabata Twiga, Kisiwani na Makuburi, walijifungia ndani kuanzia saa mbili usiku.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »